Mwongozo wa Jumuiya ya Uber
ULAYA NA KUSINI MWA JANGWA LA SAHARA
Mwongozo wetu umebuniwa kufanya kila huduma iwe salama, iheshimike na iridhishe. Unapaswa kuzingatiwa na kila mtu anayetumia mfumo wa Uber (“Mfumo wa Uber Marketplace”), ikiwa ni pamoja na wala si tu madereva, wasafiri, wasafirishaji, watumiaji wa Uber Eats, wauzaji na biashara. Unajumuisha pia mawasiliano ambayo unaweza kufanya na wafanyakazi na wakandarasi wa Uber, ikijumuisha katika Vituo vya Madereva wa Uber, kupitia mifumo ya usaidizi mtandaoni au kupitia simu.** Na, katika hali nyingine, mwongozo wetu unatumika kwa kufanya kazi nje ya Mfumo wa Uber Marketplace ambao tunafahamu, ikiwa ni pamoja na wala si tu maelezo ya mifumo mingine, wakati mienendo hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa Mfumo wa Uber Marketplace.
Asante kwa kujiunga nasi katika kusaidia na kudumisha mazingira bora.
Mwongozo ufuatao unafafanua kwa kina baadhi ya matendo ya ushirika mzuri tunayohimiza kwenye Mfumo wa Uber Marketplace na pia matendo au hali zinazoweza kukufanya upoteze uwezo wa kutumia mfumo wa Uber Marketplace. Kutakuwa na matukio yasiyotarajiwa ambayo yanaweza kusababisha upoteze uwezo wa kutumia huduma na Mfumo wa Uber Marketplace, lakini mwongozo ufuatao —ambao tutabadilisha mara kwa mara—una maelezo ya msingi ya matendo tunayotarajia kutoka kwa watu wote katika jumuiya ya Uber. Hatua ya kutofuata mwongozo wetu wowote inaweza kusababisha ukiukaji au kutotii masharti ya mkataba wako na Uber na inaweza kusababisha kupoteza uwezo wa kutumia sehemu au Mfumo wote wa Uber Marketplace.
Tafadhali chukua muda wako ili uusome.
Mwongozo wetu sote
Kila mtu anayejisajili kwenye akaunti ya Uber anatakiwa kufuata Mwongozo wa Jumuiya ya Uber. Unaonesha nguzo 3 na viwango vifuatavyo katika kila mojawapo ya sehemu hizi.
Heshimu watu wote
Jumuiya yetu ni anuwai na wakati mwingine unaweza kukutana na watu ambao huenda hawafanani nawe au wana itikadi tofauti. Mwongozo katika sehemu hii husaidia kukuza mawasiliano mazuri wakati wa kupokea kila huduma.
Tushirikiane kuimarisha usalama wa kila mmoja
Timu yetu inajitahidi kila siku ili kumpa kila mmoja huduma salama. Usalama wako ni muhimu zaidi kwetu. Kanuni hizi zilitungwa kwa sababu hii. Kando na kufuata Mwongozo huu wa jumla wa Jumuiya ya Uber, unaweza pia kupata kanuni zaidi za Uber Eats chini ya "Mwongozo wa ziada kwa wauzaji na wasafirishaji wa Uber Eats" hapa chini.
Fuata sheria
Tumejitolea kufuata sheria zote zinazotumika na kuaminika na tunatarajia kila mtu anayetumia Mfumo wa Uber Marketplace kutekeleza wajibu wake na kutii sheria na kanuni husika, pamoja na sheria na kanuni za viwanja vya ndege panapohitajika.
Maoni yako ni muhimu
Ikiwa jambo litatokea, liwe zuri au baya, tunarahisisha mchakato ili uweze kutuambia moja kwa moja kwenye App au kwa kuwasiliana na timu ya Huduma kwa Wateja wa Uber. Timu yetu inaendelea kuboresha sera na kanuni zetu, kwa hivyo maoni yako yanatusaidia kuchukua hatua inayofaa na kudumisha ubora wa kanuni zetu kadri teknolojia yetu inavyoimarika.
Heshimu watu wote
Mtendee kila mtu katika jumuiya ya Uber jinsi ungependa kutendewa: kwa heshima. Hatua unazochukua unapotumia Mfumo wa Uber Marketplace zinaweza kuathiri usalama na starehe ya wengine. Ni vyema kuwa na adabu. Ndiyo maana unatakiwa kufanya maamuzi yenye busara na kuwaheshimu watumiaji wengine wa Uber Marketplace na kutangamana na watu wengine kwenye Jumuiya ya Uber—kama vile ungefanya tu ukiwa katika maeneo ya umma.
Kwa mfano, jaribu kufika mapema wakati wa kuabiri gari na kuchukua chakula. Kwa kawaida, si vizuri kupiga kelele, kuapa au kufunga milango kwa nguvu. Na kwa kudumisha usafi—iwe ni kwa kuenda na takataka nyumbani au kupangusa kinywaji kilichomwagika, utasaidia kuhakikisha kwamba kila mtu anapata safari nzuri. La muhimu zaidi, kumbuka kwamba unapotangamana na watu wengine katika jumuiya ya Uber, unaweza kukutana na watu ambao wanaonekana kuwa tofauti na wewe au wenye mawazo tofauti na yako. Tafadhali heshimu tofauti hizo. Tunaamini kwamba kila mtu anapaswa kufurahia na kuridhishwa anapotangamana na watu wengine katika jumuiya ya Uber. Ndiyo sababu tumeweka kanuni na sera za kuhusu kugusana kimwili, dhuluma za kingono na matendo mabaya, vitisho na ujeuri, kuwasiliana baada ya safari, ubaguzi na uharibifu wa mali.
Kugusana kimwili
Usimguse mtu usiyemfahamu au mtu yeyote unayekutana naye kwenye Mfumo wa Uber Marketplace. Kuna matukio machache tu yanayoruhusiwa kwa watu wanaohitaji au kuomba usaidizi wa kimwili (kwa mfano, wasafiri wanaotumia Uber Assist ambao wanaweza kuhitaji usaidizi wa kuingia na kushuka kwenye gari) au wanapolazimika kugusana (kama vile wakati wa safari fulani za Uber Moto). Hairuhusiwi kamwe kumjeruhi au kupanga kumjeruhi mtu yeyote.
Dhuluma za kimapenzi na kukoseana heshima
Sote tunathamini nafasi na faragha yetu binafsi. Ni sawa kuchati na watu wengine. Lakini tafadhali usitoe maoni kuhusu sura ya mtu au kuuliza ikiwa hajaoa. Dhuluma za kingono na kukosea heshima ya aina yoyote zimepigwa marufuku. Matendo mabaya na dhuluma za kingono huhusu kumgusa mtu kingono bila idhini yake ya wazi.
Faragha na nafasi ya kibinafsi inapaswa kuheshimiwa. Orodha ifuatayo inatoa mifano ya baadhi ya matendo yasiyofaa, lakini haijakamilika.
- Usiulize maswali ya kibinafsi (kwa mfano, kuhusu hali ya uhusiano au mwelekeo wa ngono)
- Usitoe maoni kuhusu sura (kwa mfano, maoni ya kudunisha au “ya kinaya”)
- Usitoe maoni au ishara dhahiri (kwa mfano, maneno, ujumbe au picha za kuchochea ngono)
- Usifanye utani (kwa mfano, kutania kwa ishara au kumkaribia mtu sana)
- Usioneshe vitu visivyofaa (kwa mfano, vitu au picha zinazochochea ngono)
- Uber ina sheria ya kutoonesha maudhui ya ngono, bila kujalisha kama unamfahamu mtu huyo au hata kwa idhini yake
Vitisho na matendo ya ujeuri
Matendo ya fujo, majibizano au unyanyasaji hayaruhusiwi. Usitumie lugha, ishara au kuchukua hatua ambazo zinaweza kumkosea mtu heshima, kumtisha au zisizomfaa. Kwa mfano, usioneshe picha (kama vile zinazochochea ngono au vurugu za kimwili) kwa watu wengine katika jumuiya ya Uber; hii ni pamoja na kuonesha picha hizo bila idhini kupitia mifumo ya huduma kwa wateja wa Uber mtandaoni au kuhusiana na Mfumo wa Uber Marketplace. Unashauriwa kutojadili mada za kibinafsi ambazo zinaweza kusababisha upinzani, kama vile dini na imani za kisiasa.
Mawasiliano baada ya safari
Mawasiliano yanapaswa kuisha wakati usafirishaji watu au oda umekamilika, isipokuwa wakati wa kurudisha kitu kilichopotea. Mawasiliano yasiyotakikana yanaweza kuonekana kama unyanyasaji na hujumuisha kumtumia ujumbe mfupi, kumpigia simu, kuwasiliana katika mitandao ya kijamii, kumtembelea au kujaribu kumtembelea mtu binafsi baada ya safari au baada ya kumpelekea oda. Usitume maelezo yoyote ya mawasiliano yasiyofaa.
Ubaguzi
Unapaswa kuhisi salama na kuheshimiwa kila wakati. Ndiyo maana haturuhusu tabia au mienendo ya ubaguzi, ikijumuisha kwenye timu ya Huduma kwa Wateja wa Uber au katika Kituo cha Madereva wa Uber. Usimbague mtu kwa msingi wa sifa kama vile umri, rangi, ulemavu, utambulisho wa kijinsia, hali ya ndoa, asili ya kitaifa, ujauzito, dini, uraia, sura, rangi, dini au imani, msimamo wa kisiasa, mwelekeo wa kingono au sifa zozote zinazolindwa kwa mujibu wa sheria husika.
Kwa mfano, huruhusiwi:
- Kukataa kutoa huduma kwa sababu ya sifa kama vile umri wa mtu, rangi, ulemavu, utambulisho wa kijinsia, hali ya ndoa, ujauzito au uzazi, asili ya kitaifa, sura, rangi, dini au imani, msimamo wa kisiasa, mwelekeo wa kingono au sifa nyingine zinazolindwa kwa mujibu wa sheria husika. Sheria za nchi husika zinaweza kumtaka/au kuruhusu kutoa huduma kwa na pia kwa manufaa ya kundi mahususi la watu. Katika maeneo hayo, huduma zinazotakiwa au kuruhusiwa kwa mujibu wa sheria na vigezo husika zinakubaliwa chini ya mwongozo huu.
- Kutathmini mtumiaji mwingine—iwe ni madereva, wasafiri, wasafirishaji, watumiaji wa Uber Eats, wauzaji, migahawa au biashara—kulingana na sifa hizi.
- Ubaguzi kulingana na mahali msafiri anakoenda au mahali mtumiaji wa Uber Eats anapopelekewa chakula. Tunaelewa kuwa usafirishaji abiria au oda ni mojawapo tu ya shughuli muhimu katika mtindo wako wa maisha. Si kinyume cha mwongozo kukataa kusafirisha watu au oda iwapo shughuli hiyo haikufai. Huruhusiwi kukataa au kughairi, au kutumia vipengele vya Mfumo wa Uber Marketplace kimakusudi kuzuia maombi ya kusafirisha watu au oda ili kuepuka eneo fulani kwa ajili ya tabia za watu au biashara zinazoendelezwa katika eneo hilo.
Pata maelezo zaidi kuhusu sera ya Uber Dhidi ya Ubaguzi hapa.
Tunataka pia kuongeza chaguo za usafiri na huduma kwa watu wenye ulemavu. Ndiyo maana tuna maelezo kwa madereva, wasafiri na watumiaji wa Uber Eats kuhusu mada hii. Unaweza kwenda hapa ili upate maelezo zaidi kuhusu ahadi ya Uber ya ufikiaji. Madereva wanaotumia Mfumo wa Uber Marketplace wanapaswa kuzingatia sheria zote zinazosimamia usafirishaji wa watu walio na ulemavu, ikiwa ni pamoja na kusafirisha wanyama wa kutoa huduma na vifaa vya kuwasaidia (kama vile viti vya magurudumu).
Uharibifu wa mali
Huruhusiwi kamwe kuharibu mali. Baadhi ya mifano inajumuisha kuharibu gari au chombo kingine cha usafiri ulichoitisha kupitia Mfumo wa Uber Marketplace, kuvunja au kuharibu simu au tableti, kumwaga chakula au kinywaji kimakusudi ndani ya gari, kuvuta sigara kwenye gari, kuharibu eneo la muuzaji au kutapika kwa sababu ya ulevi au vinginevyo. Ukiharibu mali, utawajibikia gharama ya kuisafisha na kuikarabati, bila kujumuisha uharibifu wa kawaida unaosababishwa na matumizi.
Tushirikiane kuimarisha usalama wa kila mmoja
Kila mtu ana wajibu wa kutekeleza ili kuhakikisha mazingira salama. Ndiyo maana tuna kanuni za kuzingatia wakati wa kutumia akaunti pamoja, umri wa mmiliki wa akaunti na mengineyo.
Kutumia akaunti pamoja
Huruhusiwi kutumia akaunti pamoja na wengine. Ili utumie Mfumo wa Uber Marketplace, unafaa kusajili na kuwa na akaunti yako mwenyewe inayofanya kazi. Usimruhusu mtu mwingine atumie akaunti yako na usioneshe mtu mwingine maelezo yako ya kibinafsi yanayotumiwa kwenye akaunti yako, ikiwa ni pamoja na wala si tu jina la mtumiaji, nenosiri au picha zako, kwa mtu mwingine ili kuingia kwenye Mfumo wa Uber Marketplace. Kwa mfano, watu wanaosafirisha chakula sharti wakamilishe mchakato wote wa usafirishaji wenyewe—ikiwa ni pamoja na utunzaji wowote baada ya oda kuchukuliwa kutoka kwa muuzaji hadi kwa mteja wa Uber Eats anapopokea chakula—bila kuacha hatua yoyote.
Watu walio chini ya umri wa miaka 18
Sharti uwe na umri wa miaka 18 au zaidi ili uweze kuwa na akaunti ya Uber. Hii inamaanisha kuwa sharti uwe na umri wa angalau miaka 18 ili uendeshe gari bila kuambatana na mtu mzima. Mtu aliye na akaunti haruhusiwi kuitisha usafiri au kusafirisha chakula kwa ajili ya walio na umri wa chini ya miaka 18 bila kuambatana naye au na mtu mzima wakati wa safari au wakati wa kupokea chakula. Watoto pia hawaruhusiwi kuagiza chakula kwa kutumia akaunti ya watu wazima ya Uber Eats. Masharti haya ya umri hutumika isipokuwa kama mwongozo, vigezo na masharti au sera zetu zinasema vinginevyo.
Wasafiri wa ziada na wasio na akaunti
Unapoendesha gari kwa kutumia App ya Uber, hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kwenye gari isipokuwa aliyeitisha usafiri pamoja na wageni wake. Mwongozo huu unatumika isipokuwa tu vigezo na masharti ya mwongozo au sera zetu ziseme vinginevyo. Mmiliki wa akaunti atawajibikia matendo ya wasafiri wenzake wakati wote wa kusafiri kwenye Uber. Ukiitisha usafiri au kusafirisha oda kwa niaba ya mtu mzima, utawajibikia matendo yake wakati wa usafirishaji.
Maelezo ya gari
Ili kurahisisha kuchukuliwa au kusafirisha chakula, Mfumo wa Uber Marketplace huwapa wasafiri na wateja wa Uber Eats taarifa za kuwatambulisha madereva na wasafirishaji pamoja na magari yao, ikiwemo namba pleti, aina na muundo wa gari, picha ya wasifu na jina lake. Maelezo yasiyo sahihi au ambayo muda wake umeisha huwakanganya wasafiri na wateja wa Uber Eats na yanaweza kuathiri vibaya huduma yao ya kutumia Mfumo wa Uber Marketplace.
Madereva na wasafirishaji wa chakula wanapaswa kukamilisha usafirishaji wa watu au oda kwa kutumia magari yaliyoidhinishwa pekee. Ili tuweze kukupa maelezo sahihi, tujulishe maelezo ya gari lako na mabadiliko yoyote kwenye hati zako ambayo huenda yakasababisha tatizo, kama vile leseni ya udereva ambayo muda wake unakaribia kuisha.
Mikanda ya usalama
Mikanda ya usalama inaweza kuwa njia bora zaidi ya kuokoa maisha na kupunguza majeraha yanayotokana na ajali za barabarani. Kila dereva, msafirishaji au msafiri, hata aliye kwenye kiti cha nyuma, sharti afunge mkanda wa usalama kila wakati. Wasafiri wanapaswa kuitisha gari ambalo lina viti vya kutosha idadi yao na wasisafiri katika makundi makubwa yanayozidi idadi ya mikanda ya usalama kwenye gari. Madereva wanaweza kukataa safari ikiwa hakuna mikanda ya usalama ya kutosha kila msafiri kwenye gari lake.
Helmeti kwa ajili ya baiskeli, mopedi na skuta
Kwa usalama wako, unaposafiri kwa baiskeli, mopedi au skuta, hakikisha una helmeti inayokutosha vizuri. Helmeti inaweza kukulinda ukiivaa vizuri kulingana na maelekezo ya mtengenezaji, kwa mfano ifunike kipaji chako cha uso na uifungie chini ya kidevu chako.
Matumizi ya kamera ya dashibodi zinazorekodi video na/au sauti
Madereva wanaweza kuchagua kusakinisha na kutumia kamera ya dashibodi, ambayo inaweza kutumika kurekodi safari na kutoa ushahidi kwa Uber, mamlaka ya kutekeleza sheria au kampuni za bima endapo kutatokea hitilafu kwenye safari. Tafadhali kumbuka yafuatayo:
- Wasafiri wanaoabiri gari la usafiri wa pamoja lenye kamera ya dashibodi wanaweza kuwa na wasiwasi kuhusu jinsi video, picha au mazungumzo yaliyorekodiwa na kamera ya dashibodi yatakavyotumika. Katika baadhi ya maeneo, sheria na kanuni zinamhitaji msafiri kutoa idhini ya kurekodiwa. Tafadhali angalia sheria za eneo lako ili uelewe majukumu yako.
- Madereva wanaweza kutuma rekodi kwa Uber kwa hiari yao. Uber itakagua video zilizowasilishwa na kuchukua hatua kulingana na Mwongozo wa Jumuiya na sheria na masharti ya mfumo.
Kuonesha au kutiririsha picha, sauti au rekodi ya video ya mtu kwenye mitandao ya kijamii au katika maeneo mengine ya kidijitali au ya umma, ni ukiukaji wa Mwongozo wa Jumuiya yetu na unaweza kusababisha uchunguzi zaidi kutoka kwa timu yetu ya usalama.
Tahadhari
Hatua ya kuwa barabarani ina maana kwamba una jukumu la kuhakikisha usalama wako na watu wengine. Hii inamaanisha kuwa mwangalifu barabarani na kupumzika vizuri, ili uweze kushughulikia hali yoyote kwa haraka. Tunakagua ripoti za ajali na mienendo isiyo salama ya kuendesha gari.
Usimamizi na utunzaji mzuri
Kwa mujibu wa vigezo vya mkataba wa Uber, madereva na wasafirishaji wanatakiwa kukagua magari mara kwa mara na kuhakikisha kuwa yako katika hali nzuri, ikiwa ni pamoja na wala si tu breki, mikanda ya usalama na magurudumu. Hii inamaanisha kudumisha magari yao kulingana na viwango vya usalama na matengenezo vya sekta, na kufuatilia na kukarabati sehemu zozote ambazo zimebainishwa na mtengenezaji.
Kutumia barabara pamoja
Hali ya kudumisha usalama barabarani inawataka madereva wazingatie matendo salama, yanayojumuisha kuwajali wasafiri wote, bila kubagua njia wanazotumia kusafiri.
Matukio ya dharura
Uber inaweza kuchukua hatua zaidi ili kujaribu kudumisha usalama wa mfumo wetu wakati wa dharura za umma, ikijumuisha majanga ya kiasili, dharura za afya ya umma na mikasa ya umma.
Kwa mfano, Uber ikipokea habari kutoka kwa mamlaka ya afya ya umma kwamba mtu anayetumia Mfumo wa Uber Marketplace anaweza kudhuru umma, tunaweza kusitisha akaunti ya mtu huyo hadi itakapokuwa salama kabla ya kumruhusu aendelee kutumia Mfumo wa Uber Marketplace. Vivyo hivyo, tunaweza kuwazuia watu katika jiji au eneo zima wasitumie sehemu au Mfumo wote wa Uber Marketplace au kuweka masharti mengine kwa mujibu wa mwongozo wa mamlaka wakati wa dharura ya afya ya umma, majanga ya kiasili au mikasa mingine ya umma. Au, wakati utumiaji wa wa mfumo Uber unaweza kusababisha hatari.
Mwongozo wa ziada kwa wauzaji na wasafirishaji wa Uber Eats
Mbali na kufuata Mwongozo wote wa Jumuiya ya Uber, watumiaji wa mfumo wa Uber Eats sharti wafuate masharti yaliyo hapa chini yanayotumika katika oda na usafirishaji wa Uber Eats.
Utunzaji sahihi wa oda (taarifa kwa wauzaji)
Wauzaji wanapaswa kutimiza masharti yote ya leseni na kanuni na sheria nyingine zote za usalama wa vyakula - zikiwemo kanuni za usafi na usalama wa chakula, pamoja na mbinu bora za sekta na sera za Uber. Wauzaji ni sharti wawe na leseni na/au vibali halali panapohitajika kisheria.
Vyakula vingi vinavyopikwa huharibika haraka na vinaweza kusababisha magonjwa kama havitatunzwa vizuri. Vyakula kama hivi vinaweza kudhuru afya visipowekwa kwa muda na hali joto inayostahili kabla ya kuchukuliwa.
Ili kusaidia kuhakikisha kuwa chakula kinawafikia watumiaji wa Uber Eats kikiwa salama, tunahimiza wauzaji wafungashe vizuri kabla ya kusafirisha. Wauzaji wanatarajiwa kuzingatia maelezo wanayopewa na watumiaji wa Uber Eats yanayohusu mizio ya chakula, vyakula visivyokubaliwa au masharti mengine ya lishe na wasikubali maombi ya oda ambayo hawawezi kutii.
Usafirishaji sahihi wa oda (taarifa kwa wasafirishaji)
Migahawa inaweza kutunga mwongozo maalum wa usafirishaji unaohimiza usalama wa chakula, kuzingatia mwongozo wa kanuni au kukidhi masharti ya lishe ya mtumiaji wa Uber Eats. Kwa mfano, wauzaji wanaweza kumwarifu msafirishaji atenganishe vyakula Halal na visivyo Halal. Wasafirishaji wanapaswa kufuata mwongozo kama huo kutoka kwa wauzaji kila wakati.
Msafirishaji anayetumia mkoba wa kuhifadhia chakula anaweza kumpa mteja huduma bora zaidi ya Uber Eats, lakini si lazima autumie, isipokuwa kama anasafirisha katika eneo ambalo sharti utumike. Usafirishaji kwa kutumia baiskeli ni bora zaidi ukitumia mkoba maalum ili kulinda chakula dhidi ya kunesanesa na hali ya anga.
Wasafirishaji wanapaswa kusafirisha oda kwa usalama na kulingana na kanuni husika za usalama. Kwa mfano, hawapaswi kuharibu au kufungua vifurushi wakati wa usafirishaji.
Jinsi ambavyo wauzaji wanaweza kudumisha mazingira salama ya kuchukua oda
Wauzaji na wafanyakazi wao wanatakiwa kufanya maamuzi bora na kuwatunza vizuri wasafirishaji ili kuwafanya wahisi vizuri, jinsi wanavyowachukulia wateja wao binafsi. Pia, wanapaswa kuwa na eneo salama la kuchukua oda; kwa mfano, wauzaji wanapaswa kujitahidi kuzuia matukio ya vurugu kwenye maeneo ya biashara ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa wasafirishaji.
Usafirishaji wa pombe
Sharti oda zote zilizo na pombe zizingatie vigezo na masharti yanayotumika ya usafirishaji wa pombe na saa za kazi. Watumiaji wa Uber Eats walio na umri unaoruhusiwa kununua pombe na ambao hawajalewa ndio tu wanaoweza kuagiza na kupokea oda za pombe panapohitajika. Watumiaji wa Uber Eats wataombwa kuonesha vitambulisho vya picha vilivyotolewa na serikali ili kuthibitisha umri na utambulisho wakati wa kupokea pombe. Ikiwa mtumiaji wa Uber Eats hana kitambulisho sahihi cha picha kilichotolewa na serikali, au anaonekana kuwa amelewa, hatakabidhiwa oda ya pombe na inaweza kurudishwa kwa muuzaji kwa niaba ya mtumiaji wa Uber Eats kwa gharama ya mteja husika wa Uber Eats. Watumiaji wa Uber Eats hawawezi kuweka oda ya pombe ipelekwe kwenye sehemu ya umma ambapo haparuhusu vifaa vifunguliwe, au katika maeneo mengine yoyote ambayo hayaruhusu kubeba au kunywa pombe.
Kudumisha huduma bora kwa matarishi na watumiaji wa Uber Eats
Ni muhimu wauzaji waheshimu wasafirishaji na watumiaji wa Uber Eats. Wauzaji wanapaswa kuwa makini ili kutayarisha na kuweka vyakula sahihi katika oda ya mteja wa Uber Eats. Mteja wa Uber Eats akipokea bidhaa zisizofaa, inaweza kusababisha huduma mbaya.
Kuchukua muda mrefu kuandaa chakula, muda mrefu kuchukua oda (muda anaochukua msafirishaji kuingia na kutoka kwenye eneo la mfanyabiashara akiwa na oda, ikiwa ni pamoja na muda wa kusubiri), muda wa chini wa mtandaoni (muda wa muuzaji kupatikana mtandaoni), kuchukua muda mrefu kabla ya kukubali oda na viwango vya juu vya kughairi pia huwapa huduma mbaya watumiaji na wasafirishaji wa Uber Eats.
Ikiwa vipimo hivi, au vingine, ni vibaya zaidi kuliko wastani wa mji wa muuzaji, vinaweza kuathiri vibaya huduma za washirika wengine kwenye mfumo wa Uber Eats, kwa hivyo vipimo vya muuzaji vinapaswa kuwa angalau wastani wa mji wake. Ikiwa vipimo vya muuzaji viko chini ya kiwango cha chini zaidi, tutamjulisha.
Bidhaa zilizopigwa marufuku
Wauzaji wanaweza tu kutoa bidhaa za mauzo moja kwa moja kulingana na makubaliano yao na Uber. Huruhusiwi kuweka bidhaa maalum zinazodhibitiwa au zisizo halali, kulingana na sheria na kanuni husika, kwenye menyu ya Uber Eats ya muuzaji. Uber inaweza kuondoa—au vinginevyo kuzuia uwezo wa muuzaji kuchapisha kwenye—menyu ya Uber Eats ya muuzaji, bidhaa zozote ambazo Uber inachukulia kuwa zimepigwa marufuku au hazifai.
Fuata sheria
Tuna masharti kulingana na sheria na kanuni zinazotumika ambazo kila mtu anapaswa azifuate. Kwa mfano, kutumia Mfumo wa Uber Marketplace kutekeleza uhalifu wowote— kama vile kusafirisha dawa za kulevya, utengenezaji wa pesa bandia, usafirishaji haramu wa dawa za kulevya au binadamu—au kukiuka sheria au kanuni nyingine yoyote, imepigwa marufuku kabisa.
Fuata sheria zote
Kila mtu ana wajibu wa kujua na kutii sheria zote husika, ikiwa ni pamoja na sheria na kanuni za viwanja vya ndege ukiwa katika uwanja wa ndege na sheria za barabara— ikiwa ni pamoja na kutii sheria za trafiki, alama na ishara—wakati wote unapotumia Mfumo wa Uber Marketplace.
Muda wa matumizi ya leseni, vibali na hati zingine zozote za kisheria zinazohitajika kwa madereva na wasafirishaji haupaswi kuwa imeisha. Kwa mfano, madereva na wasafirishaji wote wanaotumia magari wanatakiwa kisheria kuwa na leseni, bima halali ya dereva na hati ya usajili wa gari. Hali hii inajumuisha kutimiza masharti yote ya kusafiri pamoja au kukodisha dereva katika eneo lako. Tunakagua ripoti za ajali au matatizo ya trafiki ambayo huenda yametokea wakati wa kusafirisha watu au oda na ripoti nyingine, zikiwemo zile ambazo zinaweza kuonesha uendeshaji mbaya au usio salama. Sheria za nchini zinazohusu maegesho zinaweza kukuzuia kuegesha gari katika baadhi ya maeneo unapochukua oda, kusafirisha oda au kusubiri wasafiri wawasili au washuke. Kwa mfano, ni kinyume cha sheria kufunga njia za baiskeli au kufunga njia za walio na ulemavu.
Kwa wasafiri na watumiaji wa Uber Eats, mruhusu dereva au msafirishaji aendeshe gari. Kwa mfano, msafiri hapaswi kugusa usukani, au gia au vinundu, vitufe au vifaa vingine ambavyo vinatumika kuendesha gari. Kwa wasafiri na watumiaji wa Uber Eats, usimwombe dereva au msafirishaji kuongeza kasi au kusimama, kushukisha au kupitia mahali pasiporuhusiwa.
Unapoendesha au kuegesha baiskeli, mopedi au skuta, zingatia kanuni na sheria za mahali ulipo. Kufuata sheria za barabarani kwa kawaida hukuhitaji uwapishe watu wanaotembea kwa miguu, kuendesha upande unaofaa, kuonyesha ishara ikiwa unanuia kupiga kona, na kusimama kabisa kwenye taa nyekundu na alama za kusimama.
Viti vya watoto
Madereva na wasafiri wanapaswa kutii sheria husika wanapowasafirisha watoto. Pale ambapo sheria inataka utumiaji wa kiti cha mtoto, ni jukumu la msafiri kutoa na kuweka kiti kinachofaa, isipokuwa kama mwongozo, vigezo na masharti au sera zetu zinasema vinginevyo. Watoto walio na umri wa chini ya miaka 12 wanapaswa kuketi kwenye viti vya nyuma.
Unapowachukua wasafiri walio na watoto wadogo, unaweza kuwapa muda zaidi kuweka kiti cha mtoto vizuri kabla ya kuanza kuendesha gari. Ikiwa msafiri hana kiti cha mtoto kinachofaa, ikiwa dereva hangependa msafiri aweke kiti cha mtoto kwenye gari lake, ikiwa mtoto haonekani kutimiza masharti ya kimo na uzani wa usalama wa kiti, au ikiwa dereva anahisi kwamba mtoto hawezi kubebwa kwa usalama, dereva anaweza kughairi safari.
Wanyama wa kutoa huduma na vifaa vya usaidizi
Madereva wanaotumia App ya Uber Driver hawapaswi kumkataa msafiri aliye na mnyama wa kutoa huduma au kifaa cha kumsaidia (kama vile kiti cha magurudumu au mikongojo) kwa sababu ya hali hizo. Kwa kawaida, sheria zinazotumika huwakataza madereva kuwanyima wasafiri huduma kwa sababu ya wanyama au vifaa vya kuwasaidia, na kuwabagua wasafiri walio na wanyama wa kutoa huduma au vifaa vya kuwasaidia, hata kama dereva ana imani tofauti ya kidini au anaogopa wanyama. Kukataa kimakusudi kumsafirisha mtu kwa sababu ana mnyama wa kutoa huduma au vifaa visaidizi kutasababisha kupoteza uwezo wa kufikia Mfumo wa Uber Marketplace isipokuwa panaporuhusiwa kisheria.
Pombe na dawa za kulevya
Huruhusiwi kutumia dawa za kulevya wala kufungua vifaa vya pombe ukitumia Mfumo wa Uber Marketplace.
Ikiwa wewe ni dereva au msafirishaji, kwa mujibu wa sheria huwezi kuendesha gari au baiskeli ukiwa umelewa. Sheria haikuruhusu kuendesha gari au baiskeli ukiwa umekunywa pombe, dawa za kulevya au vileo vingine ambavyo hupunguza uwezo wako wa kuendesha gari au baiskeli kwa njia salama. Ukikumbana na msafiri aliyelewa kupita kiasi au mwenye vurugu, una haki ya kukataa safari kwa sababu ya usalama wako.
Ikiwa wewe ni msafiri na una sababu ya kuamini kuwa dereva wako ni mlevi au ametumia dawa za kulevya, mwambie aghairi safari hiyo mara moja. Kisha shuka na upige simu kwa mamlaka ya karibu au huduma za dharura. Ukishuka gari lako, tafadhali pia ripoti kuhusu tukio lako kwa Uber.
Marufuku ya bunduki
Wasafiri na wageni wao, na pia madereva na wasafirishaji, hawaruhusiwi kubeba silaha wanapotumia Mfumo wa Uber Marketplace, kwa mujibu wa sheria husika. Unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu Sera yetu ya Kukataza Bunduki hapa.
Ulaghai
Udanganyifu unaweza kuvunja uaminifu na pia ni hatari. Hairuhusiwi kutoa maelezo ya uongo kwa makusudi au kutumia utambulisho wa mtu mwingine, kwa mfano wakati wa kuingia katika akaunti au kufanyiwa ukaguzi wa usalama. Ni muhimu kutoa maelezo sahihi unaporipoti matukio, kufungua na kutumia akaunti zako za Uber, kupinga matozo au ada na kuomba mikopo. Omba tu ada, matozo au kurejeshewa pesa unazostahiki, na utumie ofa na matangazo kama tu ilivyokusudiwa. Usifanye miamala isiyo sahihi kimakusudi.
Shughuli za ulaghai pia zinaweza kujumuisha: wala si tu: kuongeza muda au umbali wa safari kwa makusudi kwa sababu za ulaghai au vinginevyo; kukubali maombi ya usafiri, oda au kusafirisha oda bila nia ya kuyakamilisha, ikiwa ni pamoja na kuwashawishi wasafiri au watumiaji wa Uber Eats kughairi kwa sababu za ulaghai; kufungua akaunti bandia kwa sababu za ulaghai; kudai ada au matozo kwa ulaghai, kama vile ada za usafishaji zisizo za kweli; kuomba, kukubali au kukamilisha safari kwa ulaghai au uwongo kwa makusudi; kudai kukamilisha usafirishaji bila kuchukua oda yoyote; kuchukua oda lakini kubaki na sehemu au oda yote; vitendo vinavyokusudiwa kuvuruga au kuathiri utendaji wa kawaida wa Mfumo wa Uber Marketplace, ikiwa ni pamoja na kurekebisha mipangilio kwenye simu ili kuzuia utendaji wa mfumo na GPS; kutumia vibaya ofa na/au kutozitumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa; kupinga ada au matozo kwa sababu za ulaghai au zisizo halali; kufungua akaunti zinazofanana; au kutoa hati, rekodi au data nyingine kwa sababu za ulaghai.
Kuita wasafiri barabarani na kuchukua wasafiri nje ya mfumo
Ili kuimarisha usalama wa kila huduma, huruhusiwi kuchukua wasafiri nje ya App. Sheria inakataza kuita wasafiri barabarani unapotumia Mfumo wa Uber Marketplace, kwa hivyo usiwahi kuomba au kukubali malipo nje ya Mfumo wa Uber Marketplace. Wasafiri na watumiaji wa Uber Eats hawapaswi kulipia safari au oda kwa pesa taslimu, na wasafiri hawapaswi kuitisha usafiri kwa madereva walio nje ya Mfumo wa Uber Marketplace.
Shughuli zisizokubalika
Usitumie kamwe chapa ya biashara au hakimiliki ya Uber bila ruhusa. Ikiwa inahitajika kwa mujibu wa sheria za nchi husika kuonesha bidhaa zenye chapa ya Uber, madereva na wasafirishaji wanapaswa kutumia bidhaa zenye chapa kutoka Uber pekee. Madereva na wasafirishaji hawapaswi kuonesha bidhaa zilizo na chapa ya Uber wakiwa nje ya mfumo wa Uber. Madereva na watu wasafirishaji pia wanapaswa kurudisha bidhaa zilizo na chapa ya Uber kwenye Uber iwapo wamezuiwa kutumia mfumo. Matumizi ya bidhaa za kampuni nyingine ambazo haziruhusiwi—kama vile taa, mabango, ishara au bidhaa sawa na hizi zenye jina la Uber au alama yake ya biashara—yanaweza kuwakanganya wasafiri au watumiaji wa Uber Eats.
Maoni yako ni muhimu sana
Tumekurahisishia mchakato wa kuripoti jambo likitokea, liwe zuri au baya. Timu yetu inaendelea kuboresha viwango vyetu na maoni yako yanatusaidia kudumisha ufaafu wa viwango vyetu kadri teknolojia yetu inavyoimarika. Tafadhali kadiria huduma unayopata mwishoni mwa kila safari. Maoni ya ukweli husaidia kuhakikisha kwamba kila mtu anawajibikia vitendo vyake. Uwajibikaji huu husaidia kudumisha mazingira salama na yenye heshima. Na kitu kikitokea— kama vile ajali ya barabarani—na ungependa kuripoti, unaweza kubonyeza Usaidizi kwenye App au utembelee help.uber.com ili timu ya Huduma kwa Wateja iweze kufuatilia. Ikiwa kuna dharura au ukipata hatari ya ghafla, julisha mamlaka ya eneo lako au huduma za dharura kabla ya kuarifu Uber.
Tathmini
Madereva, wasafiri, wasafirishaji, watumiaji wa Uber Eats na wauzaji wanaweza kutoa na kupokea tathmini, na pia kutoa maoni kuhusu jinsi safari au usafirishaji ulivyofanyika. Mfumo huu wa maoni huboresha uwajibikaji na husaidia kudumisha mazingira ya heshima, usalama na uwazi kwa kila mtu. Madereva na wasafirishaji wanaweza kuona tathmini zao za sasa kwenye App. Wauzaji wanaweza kupata tathmini yao ya watumiaji na wasafirishaji wa Uber Eats kwa kuingia katika akaunti ya MsimamiziwaUber Eats. Panapohitajika, msafiri anaweza kuona tathmini yake chini ya jina lake kwa kufungua App na kugusa menyu.
Panapohitajika, kuna wastani wa chini wa tathmini katika kila mji. Hii ni kwa sababu kunaweza kuwa na tofauti za kitamaduni kulingana na jinsi watu katika miji tofauti wanavyotathminiana. Madereva, wasafiri, wasafirishaji au wauzaji ambao hawajatimiza viwango vya chini vya tathmini ya miji yao wanaweza kupoteza idhini ya kufikia sehemu au Mfumo wote wa Uber Uber Marketplace. Ikiwa tathmini zako zinakaribia kikomo hiki, tutakujulisha na tunaweza kukutumia maelezo yanayoweza kukusaidia kuboresha tathmini yako.
Kama ungependa kudumisha wastani wa tathmini za juu, ni muhimu uwe na nidhamu na heshima kwa watu wote unapotumia Mfumo wa Uber Marketplace na kushirikiana na watu wengine katika jumuiya ya Uber. Kwa kawaida madereva na wasafirishaji wanaotumia Mfumo wa Uber Marketplace hutoa huduma bora kwa wasafiri na watumiaji wa Uber Eats, na wasafiri, wasafirishaji na watumiaji wa Uber Eats wana nidhamu na heshima, kwa hivyo safari nyingi hufanyika vizuri. Kuwasiliana na huduma kwa wateja hakutasababisha kuondolewa kwa tathmini ya mtu binafsi. Tunajua kwamba wakati mwingine usafirishaji wa watu au oda hautekelezwi vizuri—ndiyo maana tathmini yako huwa wastani.
Ikiwa wewe ni dereva na umepoteza idhini ya kutumia akaunti yako ya Uber kwa sababu ya tathmini za chini, unaweza kupata fursa ya kurejea barabarani ukitimiza vigezo na kutoa uthibitisho kwamba umekamilisha kozi ya kuimarisha ubora inayotolewa na wataalamu wengine. Wasiliana na timu ya Huduma kwa Wateja wa Uber, tembelea Kituo cha Madereva wa Uber, au help.uber.com ili upate maelezo zaidi.
Kukubali Usafirishaji, oda na safari
Ikiwa wewe ni msafirishaji au dereva na hungependa kukubali maombi ya kusafirisha oda au wasafiri, unaweza kuondoka mtandaoni au kwenye akaunti. Ikiwa wewe ni muuzaji, tumia kipengele cha ‘Sitisha Oda Mpya’ au uondoe upatikanaji wa bidhaa mahususi. Hatua hii husaidia kuhakikisha kwamba mfumo unamnufaisha kila mtu.
Kwa wasafirishaji, madereva na wauzaji, ukikataa maombi ya safari au oda mfululizo, teknolojia yetu inaweza kuchukulia kwamba hungependa kukubali safari au oda zaidi au umesahau kuondoka kwenye akaunti na huenda ukaondolewa kwa muda. Hata hivyo, una uhuru wa kuingia tena wakati wowote ukiwa tayari kukubali maombi ya safari na oda.
Jinsi Uber inavyotekeleza mwongozo wetu
Kupoteza idhini ya kutumia Mfumo wa Uber Marketplace kunaweza kuathiri maisha au biashara yako. Ndiyo maana tunaamini kwamba ni muhimu kuwa na sera zinazofafanua wazi matukio yanayoweza kufanya uzuiwe kutumia Mfumo wa Uber Marketplace. Ukikiuka vigezo vyovyote vya mkataba wako na Uber, au vigezo na sera zozote husika, ikiwemo sehemu yoyote ya Mwongozo huu wa Jumuiya au sera na viwango vya ziada ambavyo tunakujulisha mara kwa mara, unaweza kupoteza uwezo kiasi au wote wa kutumia Mfumo wa Uber Marketplace. Ikiwa una zaidi ya akaunti moja za Uber, kama vile akaunti ya msafiri na ya dereva, ukiukaji wa Mwongozo wa Jumuiya pia unaweza kusababisha upoteze uwezo wa kutumia akaunti zote za Uber. Ikiwa unaamini kwamba kuna hitilafu iliyofanya usiweze kutumia akaunti yako, unaweza kuwasiliana na timu ya Huduma kwa Wateja wa Uber.
Uber hupokea maoni kupitia njia mbalimbali, hukagua ripoti zote zinazotumwa kwa timu yetu ya Huduma kwa Wateja ambazo huenda zinakiuka Mwongozo wetu wa Jumuiya na tunaweza kuchunguza kupitia timu maalum. Tukifahamishwa kuhusu matendo yanayoweza kusababisha matatizo, tunaweza kuwasiliana nawe ili tuweze kuyachunguza. Tunaweza, kwa hiari yetu, kusimamisha akaunti yako au kusitisha akaunti yako hadi tutakapokamilisha uchunguzi wetu.
Ukiukaji wa sehemu yoyote ya mwongozo wetu unaweza kusababisha kuondolewa kwa uwezo kiasi au wote wa kutumia Mfumo wa Uber Marketplace. Inaweza kujumuisha ripoti za ukiukaji wa Mwongozo wetu wa Jumuiya na hatua fulani unazoweza kuchukua nje ya Mfumo wa Uber Marketplace, ikiwa ni pamoja na wala si tu maelezo ya mfumo mwingine, kama tutabaini kuwa vitendo hivyo vinatishia usalama wa jumuiya ya Uber, wafanyakazi wetu na makandarasi, au kusababisha madhara kwa chapa, sifa au biashara ya Uber. Ikiwa matukio yaliyoripotiwa yalikuwa makubwa au ya kurudiwa, au ukikataa kushirikiana, unaweza kupoteza uwezo wa kutumia Mfumo wa Uber Marketplace. Matendo yoyote yanayohusisha vurugu, unyanyasaji wa kingono, unyanyasaji, ulaghai, ubaguzi, au shughuli za udanganyifu, haramu au zisizo salama unapotumia Mfumo wa Uber Marketplace yanaweza kusababisha upoteze uwezo wa kutumia Mfumo wa Marketplace Platform. Vilevile, watekelezaji wa sheria wanapohusika, tutashirikiana nao katika uchunguzi kulingana na Mwongozo wetu wa Utekelezaji wa Sheria.
Nchi, miji na viwanja vingi vya ndege hudhibiti utoaji wa huduma fulani, zikiwemo huduma za usafiri wa pamoja, kwenye Mfumo wa Uber Marketplace. Ikiwa tutabaini kuwa akaunti yako ya dereva au msafirishaji haitii masharti husika ya kisheria, tunaweza kuondoa uwezo wako wa kutumia Mfumo wa Uber Marketplace.
Mwishowe, madereva na wasafirishaji wanaotaka kutumia Mfumo wa Uber Marketplace wanaweza kufanyiwa uchunguzi, ikiwemo ukaguzi wa rekodi ya gari na uchunguzi wa uhalifu kama inavyotakiwa. Dereva au msafirishaji atapoteza uwezo wa kutumia akaunti zake za Uber ikiwa ukaguzi wa rekodi ya gari, historia ya uhalifu au ukaguzi mwingine utagundua ukiukaji wa Mwongozo wa Jumuiya ya Uber au vigezo vingine vinavyotakiwa na wasimamizi wa eneo husika.
Ili usome maelezo zaidi kuhusu Mwongozo wetu wa Jumuiya, nenda hapa.
Wasafiri na watumiaji wa Uber Eats wanaweza kupata masharti ya Uber na Uber Eats hapa. Madereva na wasafirishaji wanaweza kupata mkataba wa kisheria na Uber hapa.
**Kumbuka: Madereva na wasafirishaji si mawakala (halisi, wa kukisiwa au vinginevyo) au wafanyakazi wa Uber. Madereva na wasafirishaji hawatekelezi mamlaka yoyote (halisi, dhahiri au vinginevyo). Ni wahudumu wa kujitegemea.
Wähle deine bevorzugte Sprache
Über uns